Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Mohammad Abdul-Salam ameashiria mapatano ya Imarati na utawala haramu wa Israel ya kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia na kusema: Jumuiya ya Nchi za Kiarabu na Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) zimepongeza na kukaribisha mapatano hayo kwa kunyamazia kimya hatua ya Imarati.
Awali Waziri wa Habari wa Serikali ya Uokovu wa Kitaifa ya Yemen, Dhaifullah al Shami alikuwa ametangaza kuwa, makubaliano ya utawala ghasibu wa Israel na Imarati ya kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia ni doa la fedheha linalopigwa vita na kulaani na kila mtu mwenye damu ya Kiarabu.
Baraza Kuu la Masuala ya Siasa la Yemen pia limetangaza kuwa limehitimisha miamala ya kibiashara ya Imarati kama hatua ya kukabiliana na usaliti uliofanywa na nchi hiyo dhidi ya watu wa Palestina.
Wakati huo huu Katibu Mkuu wa Kamati ya Utendaji ya Harakati ya Ukombozi wa Palesina (PLO) Saeb Erekat amemtaka Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu, Ahmed Aboul Gheit kutoa taarifa inayolaani hatua ya Imarati ya kuanzisha uhusiano na utawala wa Kizayuni wa Israel au ajiuzulu nafasi hiyo.
Alhamisi ya jana Rais Donald Trump wa Marekani alitangaza kufikiwa mapatano baina ya Umoja wa Falme za Kiarabu na utawala haramu wa Israel kuhusu kuanzishwa uhusiano wa kidiplomasia baina ya pande mbili. Hatua hiyo imelaaniwa na harakati zote za mapambano ya ukombozi wa Palestina.
Mshauri wa ngazi za juu wa Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina Nabil Abu Rudeineh amesema mapatano hayo ya Israel na Imarati ni usaliti kwa Quds Tukufu (Jerusalem), Msikiti wa Al Aqsa na malengo matukufu ya kupigania ukombozi wa Palestina.
342/